Friday, May 11, 2012

MECHI YA BIAFRA KIDS DHIDI YA VIJANA MUSLIM YAPANGWA KUCHEZWA JUMAPILI TAREHE 13 MEI, 2012

Ile mechi iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka hasa wanaofuatilia michuano ya Copa Coca Cola kwa walio chini ya umri wa miaka 17 kanda ya Kinondoni kati ya timu Biafra Kids na Vijana Muslim imepangwa kufanyika siku ya Jumapili tarehe 13 Mei, 2012 pale pale katika uwanja wa Mwl. Nyerere, Magomeni Makurumla.
Kikosi Kazi cha Biafra Kids

Mtanange huo ambao unatarajiwa kuanza saa 4:00 asubuhi, unatarajiwa kuhudhuriwa na wanamichezo wa zamani hasa wachezaji wa soka ambao tangu kuanza kwa mashindano haya wamekuwa wakiifuatilia kwa karibu sana timu ya Biafra Kids ambao wamekuwa tishio kwa timu wanazokutana nazo.
Wachezaji, viongozi, wanachama na mashabiki wa Biafra Kids katika picha ya pamoja

Akiizungumzia mechi hiyo hasa katika upande wa maandalizi, kocha wa Timu hiyo ndugu William John ambaye anasaidiana na golikipa maarufu wa zamani katika wilaya Kinondoni Suleiman Bwato alitanabaisha kwamba, vijana wake wamejiandaa vya kutosha kwa kufanya mazoezi ya nguvu na pia kisaikolojia wameweza kukutana mara kwa mara na viongozi wa klabu yao na kuwapa hamasa ya ushindi.

Beki wa Biafra Kids Abdulkareem Moshi (katikati)

Beki machachari wa timu hiyo Abdulkareem Moshi (pichani juu) alitanabaisha kwamba amerejea toka safari mahususi kwa ajili ya kuisadia klabu yake ipate ushindi kwenye mechi hiyo. Beki huyo pia kwa niaba ya wachezaji wenzake, aliwaomba mashabiki wa timu hiyo kuhudhuria uwanjani kwa wingi ili kuishangilia na kuiunga mkono timu yao na hatimaye iibuke na ushindi mnono.

VIONGOZI, WANACHAMA WACHEZAJI, PAMOJA NA MASHABIKI WA TIMU YA BIAFRA KIDS BADO WANASISITIZA WADAU KWA KUWAOMBA KUWAWEZESHA VIJANA HAWA VIFAA VYA MICHEZO KAMA VILE MIPIRA, KONI, JEZI ZA MECHI NA ZA MAZOEZI, N.K. 

No comments:

Post a Comment