Monday, May 21, 2012

MATUKIO BAADA YA MAZOEZI YA MBIO ZA POLE POLE KATIKA PICHA

Siku ya jumapili tarehe 20 Mei, 2012 klabu ya michezo ya Biafra ilizialika klabu za Taifa Jogging na Kawe Jogging pamoja na wadau wengine katika kufanya mazoezi ya pamoja ya mbio za pole pole 'jogging' ambazo zilianzia katika makao makuu ya klabu ya Biafra kupitia barabara ya Kawawa, Dunga, Peace, Mwin'juma, Kawawa tena na kumalizikia makao makuu ya Biafra.

Wanamichezo wakimsikiliza kwa makini Mwenyekiti wa Taifa Jogging akitoa nasaha zake

Mazoezi hayo yalihudhuriwa na wanamichezo zaidi ya mia moja hamsini kutoka Temeke pamoja na Kinondoni ambapo yaliongeza hamasa hadi kupelekea watu wengine wajumuike pamoja huku nyimbo mbalimbali za kuhamasisha wakimbiaji zikiimbwa kwa ustadi mkubwa.


wanamichezo wakiimba na kucheza klabuni


Baadhi ya viongozi wa Biafra na Taifa jogging

Mashabiki wa soka nao hawakuwa nyuma kuonyesha ushabiki wao kwa kushangilia ushindi wa klabu ya Chelsea ambayo imenyakua ubingwa wa kombe la klabu bingwa ulaya kwa kuitandika sawasawa timu ya byern Munich ya ujerumani kwa mikwaju ya penati.

Wanabiafra Michael Silili (wa kwanza kulia) na Editha Tungara (wa mwisho) katika picha ya pamoja na Bi. Arafa nwenzake wakiiwakilisha Taifa Jogging

Hata mashabiki wa Liverpool nao walikuwepo

Mwanabiafra Editha Tungaraza

Ismail Hamad (kushoto) na Michaele Silili (kulia)


Akizungumza baada ya kumaliza mazoezi mwenyekiti wa Taifa Jogging alieleza kuwa wamefurahishwa sana na mwaliko wa kuja kufanya mazoezi ya pamoja kwa kuwa kutembeleana huku kutaimarisha sana uhusiano baina ya klabu rafiki, hivyo alitumia pia fursa hiyo kuwaalika Wanabiafra Temeke na kufanya mazoezi ya pamoja Taifa jogging pamoja na klabu nyingine.

Friday, May 18, 2012

BIAFRA SPORTS CLUB YAZIKARIBISHA KLABU ZA JOGGING ZA KAWE NA TAIFA KUFANYA JOGGING PAMOJA

Katika kuendeleza uhusiano na ujirani mwema mwema, klabu ya michezo ya Biafra inaendeleza programu yake endelevu ya kufanya mazoezi ya pamoja na klabu mbalimbali za jogging mkoani Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla. Programu hiyo iliyoanza kabla ya klabu kusajiliwa itaendelea tena jumapili ya tarehe 20 Mei, 2012 ambapo klabu ya Taifa Jogging ya Temeke na Kawe Jogging ya Kawe mzimuni watakuwa wageni wa klabu ya Biafra.
Baadhi ya Wana-Kawe jogging

Akithibitisha wa klabu ya Kawe ndugu Lazaro alieleza kuwa ni fursa nzuri kwa wanamichezo kukutana kwa apmoja mara kwa mara na kubadilishana mawazo pamoja na uzoefu wa namna ya kuziendeleza klabu zetu.

Klabu ya Biafra inawakaribisha wakaazi wote wa Kinondoni hasa wapenda mazoezi katika kufanya mazoezi ya pamoja siku hiyo n siku nyingine. 

Thursday, May 17, 2012

MCHEZAJI NGULI WA ZAMANI YA TIMU YA TAIFA NA YANGA KUTEMBELEA MAZOEZI YA BIAFRA KIDS

Katika harakati za kuwapa fursa za kujifunza toka kwa wachezaji wa mpira wa miguu wa zamani, klabu ya Biafra imeanzisha programu maalumu ya kuwakutanisha wachezaji wa zamani na vijana hao. Programu hiyo inayoitwa 'inspired by the legends' itaanza rasmi juma hili na itafanyika takriban mara mbili kila mwezi.
mchezaji nguli (legend) mwenye bahati ya kufungua programu hiyo ni Edibiliy Jonas Lunyamila (pichani chini) ambapo atatembelea mazoezi ya Biafra Kids siku ya ijumaa tarehe 18, Mei, 2012 katika viwanja vya Biafra Kinondoni.
Edibily Jonas Lunyamila aka Lunya

Akizungumza juu ya ujio huo, kocha wa Biafra Kids William John Masika alieleza kuwa amefanya mawasiliano na mchezajihuyo na amethibitisha kuhudhuria mazoezi na baadaye kuzungumza na vijana hao. Pia atatumia fursa hiyo kutoa ushauri kwa viongozi wa namna ya kuwaendeleza vijana hao kwa kufuata misingi na miiko ya mchezo wa mpira wa miguu.

Kwa niaba ya viongozi, wanachama, wapenzi na mashabiki wa Biafra Sports Club, tnapenda kuchukua fursa hii kumkaribisha Lunyamila klabuni kwetu. Karibu sana!!!!

Sunday, May 13, 2012

THE JUNIORZ YASHINDA 2 -1 DHIDI YA VIJANA MUSLIM

Katika kusherehekea siku ya kina mama duniani (mother's day) leo, timu ya Biafra Kids almaarufu The Juniors wameichapa timu ngumu ya Vijana Muslim almaarufu 'dume' kwa mabao 2 -1 bila huruma katika michuano ya Copa Coca Cola kwa vijana walio chini ya umri wa miaka 17 kanda ya Kinondoni.
The Jrz wakipasha misuli moto kabla ya kuingia uwanjani.

Vijana Muslim nao wakipasha moto misuli kabla ya kuingia uwanjani

Dume ni moja kati ya timu zinazohofiwa sana kwenye michuano hiyo kwa kuwa ni timu yenye uzoefu wa kushiriki mashindano mbalimbali kwa muda mrefu huku The Juniorz wakiwa wageni kabisa kwenye mashindano hayo hali iliyopelekea mashabiki wengi kuipa nafasi kubwa timu ya Dume lakini katika hali ya kushangaza, The Juniorz waliwafundisha mpira Dume.

Kikosi kilichoanza - The Juniorz

Kikosi kilichoanza - Vijana Muslim


Baada ya kutandaza kandanda safi tangu sekunde ya kwanza ya mchezo, Biafra Kids walijiandikia bao la kwanza dakika ya 28 kupitia kwa winga wake machachari Babulu Nussura. Hadi mapumziko Biafra Kids walikuwa wakiongoza kwa bao 1.
Kiongozi wa Dume akiwa na majonzi ya kufungwa timu yake

Mchezo huo ambao pia ulishuhudiwa na wanasoka mbalimbali wa zamani (pichani chini) uliendelea tena kipindi cha pili ambapo timu ya Dume walijipatia bao la kusawazisha lilioleta utata ambapo wengi miongoni mwa watazamaji walilisisitiza kuwa mchezaji aliyefunga goli la Dume alikuwa ameotea na alionekana wazi kabisa kuwa ameotea. hata hivyo, The Juniorz hawakukata tamaa kabisa kwani pamoja na kuchezewa rafu nyingi hatimae waliandika bao la pili kwa njia ya penalti dakika ya 87 baada ya golikipa wa timu ya Dume kumchezea rafu mbaya kiungo machachari wa The Juniorz Hussein Tahiddin kwenye eneo la hatari. Penati hiyo iliwekwa kimiani na Rashid Sajji.
Golikipa wa zamani

Hadi mwisho wa mchezo Biafra Kids iliibuka kidedea na ushindi wa mabao 2 -1 wakiwa na pointi saba na magoli 8. Timu hiyo inarudi tena uwanjani jumatano tarehe 16 Mei, 2012 ambapo itacheza na timu ya Hanasif mchezo ambao utapigwa katika dimba la shule ya sekondari ya Muslim ambao ni uwanja wa nyumbani wa Dume.






 



HALI YA HEWA YASHUSHA IDADI YA WANA-JOGGING JUMAPILI

Hali ya hewa ya mawingu na manyunyu ya hapa na pale imesababisha wana-jogging wengi wasijitokeze kwa ajili ya kufanya mazoezi ya pamoja kama ilivyopangwa leo. Wanamichezo waliojitokeza ni wachache sana kulinganisha na majuma yaliyopita.
Wanabiafra wakiwa barabara ya Leaders kuelekea barabara ya Kinondoni


watoto nao hawako na wala hawaachwi nyuma kwenye 'jogging'


Bila kujali uchache wao, wanabiafra walifanya mazoezi kama ilivyopangwa na hatimaye walimaliza kwa kufanya 'aerobics' klabuni. Mazoezi hayo japo yalifana lakini hali ya mazingira haikuwa nzuri kutokana na eneo kubwa linatumika kufanyia mazoezi hayo kuwa na madimwi ya maji yatokanayo na mvua zinazoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wanabiafra katika mazoezi ya aerobics wakiongozwa na Noha Machaka


Baada ya kumaliza mazoezi, wanachama waliungana pamoja na moja moja walikwenda katika uwanja wa Mwl. Nyerere, Magomeni Makurumla kuishangilia timu yao ya Biafra Kids ambao walikuwa wakichuana na Vijana Muslim mchezo ambao ulimalizika kwa Biafra Kids kuichabanga bila huruma timu ya Vijana Muslim kwa mabao mawili kwa moja.


Friday, May 11, 2012

MECHI YA BIAFRA KIDS DHIDI YA VIJANA MUSLIM YAPANGWA KUCHEZWA JUMAPILI TAREHE 13 MEI, 2012

Ile mechi iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka hasa wanaofuatilia michuano ya Copa Coca Cola kwa walio chini ya umri wa miaka 17 kanda ya Kinondoni kati ya timu Biafra Kids na Vijana Muslim imepangwa kufanyika siku ya Jumapili tarehe 13 Mei, 2012 pale pale katika uwanja wa Mwl. Nyerere, Magomeni Makurumla.
Kikosi Kazi cha Biafra Kids

Mtanange huo ambao unatarajiwa kuanza saa 4:00 asubuhi, unatarajiwa kuhudhuriwa na wanamichezo wa zamani hasa wachezaji wa soka ambao tangu kuanza kwa mashindano haya wamekuwa wakiifuatilia kwa karibu sana timu ya Biafra Kids ambao wamekuwa tishio kwa timu wanazokutana nazo.
Wachezaji, viongozi, wanachama na mashabiki wa Biafra Kids katika picha ya pamoja

Akiizungumzia mechi hiyo hasa katika upande wa maandalizi, kocha wa Timu hiyo ndugu William John ambaye anasaidiana na golikipa maarufu wa zamani katika wilaya Kinondoni Suleiman Bwato alitanabaisha kwamba, vijana wake wamejiandaa vya kutosha kwa kufanya mazoezi ya nguvu na pia kisaikolojia wameweza kukutana mara kwa mara na viongozi wa klabu yao na kuwapa hamasa ya ushindi.

Beki wa Biafra Kids Abdulkareem Moshi (katikati)

Beki machachari wa timu hiyo Abdulkareem Moshi (pichani juu) alitanabaisha kwamba amerejea toka safari mahususi kwa ajili ya kuisadia klabu yake ipate ushindi kwenye mechi hiyo. Beki huyo pia kwa niaba ya wachezaji wenzake, aliwaomba mashabiki wa timu hiyo kuhudhuria uwanjani kwa wingi ili kuishangilia na kuiunga mkono timu yao na hatimaye iibuke na ushindi mnono.

VIONGOZI, WANACHAMA WACHEZAJI, PAMOJA NA MASHABIKI WA TIMU YA BIAFRA KIDS BADO WANASISITIZA WADAU KWA KUWAOMBA KUWAWEZESHA VIJANA HAWA VIFAA VYA MICHEZO KAMA VILE MIPIRA, KONI, JEZI ZA MECHI NA ZA MAZOEZI, N.K. 

BIAFRA JOGGING YATANGAZA NJIA ITAKAZOPITA JUMAPILI TAREHE 13 MEI, 2012

Kama ilivyo ada,  kila siku ya jumapili, wanachama wa Biafra pamoja na wadau wote wanaopenda kufanya mazoezi ya mbio za pole pole hukutana na kufanya mazoezi hayo kwa pamoja. Kwa kawaida mazoezi huanzia na kuishia makao makuu ya klabu pale 90 Degrees Pub Kinondoni. Akizungumza na wanachama pamoja na wadau, Katibu Mkuu wa Biafra ndugu Yahya Poli kwa niaba ya Kamati ya Ufundi, alitangaza njia zitakazotumika kwa ajili ya mazoezi ya mbio za pole pole zitakazofanyika jumapili tarehe 13 Mei, 2012 kuanzia saa 12:30 asubuhi.
Wanabiafra wakikatiza barabara ya Ali Hassan Mwinyi

Katibu Mkuu huyo alibainisha kwamba, wanachama pamoja na wadau wote wanatakiwa kuwa klabuni kabla ya saa 12:25 asubuhi na itakapotimu saa 12:30 mazoezi yataanza moja kwa moja kwa kupitia barabara ya Kawawa kuelekea Moroko, kisha wakimbiaji wataingia barabara ya Ali Hassan Mwinyi mpaka njia panda ya kuelekea Leaders Club, wataifuata barabara hiyo hadi makutano ya barabara ya Kinondoni kuelekea shule ya sekondari Muslim, kisha watakatiza barabara ya kuelekea stereo kupitia kanisa la Pinda hadi studio. Baada ya kufika studio, wanabiafra wataifuata barabara ya Kawawa kuelekea mkwajuni hadi chuo cha Baraka na kukatiza maeneo ya Mango Garden hadi kwa Manyanya na kumalizia mbio klabuni. 
Wanabiafra wakiingia barabara ya Kawawa 

Akiongezea, Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ndugu Michael Silili  (pichani chini) alitanabaisha kwamba ruti hiyo inaweza kuwachukua wakimbiaji takriban dakika tisini kuimaliza hivyo amewasisitizia wanamzoezi wote kuwahi mapema. 
Wenyeviti - Michael Silili Mwenyekiti wa kamati ya Ufundi (kushoto) akiwa na Mwenyekiti wa Klabu Abdul Mollel

Mwenyekiti wa klabu ndugu Abdul Mollel kwa kumalizia aliwakaribisha watu wote wenye kupenda kufanya mazoezi ya mbio za pole pole kujumuika pamoja na wanachama kila jumapili na pia watumie fursa hiyo kuielewa klabu na hatimaye wajiunge na kuwa wanachama. Aliendelea kubainisha kuwa, kwa yeyote atakayependa kufanya hivyo basi awasiliane moja kwa moja na Katibu kwa simu (0715 253 653)

WE! WE! MAZOEZI NI AFYA, ACHA KUJIACHIA!!!!!!!!!!

Monday, May 07, 2012

MCHANGANI FC YALAZIMISHA SULUHU

Ile mechi iliyohairishwa kwa zaidi ya mara tatu kati ya Biafra Kids aka The Juniors dhidi ya Mchangani FC hatimaye imechezwa jana jumapili tarehe 04 Mei, 2012 saa 4:30 asubuhi katika uwanja wa Mwl. Nyerere, magomeni Makurumla.

The Juniorz wakipasha misuli kabla ya kuingia uwanjani


The Juniorz wakisalimiana na wachezaji wa Mchangani FC kabla ya kuanza kwa mechi

Mechi ilichelewa kuanza kwa takribani nusu mara baada ya kukosekana kwa mpira. Si waandaaji, Mchangani FC wala BIafra Kids waliokuwa na mpira hali iliyosababisha uazimwe mpira ambao haukuwa na bora kwa ajili ya kuchezewa mechi.

Kikosi kilichoanza cha The Juniorz

Kikosi kilichoanza cha Mchangani FC


Baada ya kupulizwa kipenga hca kuashiria kuanza kwa mechi hiyo, The Juniorz walilishambulia lango la Mchangani na kukosa magoli mawili mapema tu dakika ya 8 na ya 17. Kosa kosa hizo zilitokana na ubovu wa mpira. Pamoja na ubovu wa mpira huo, vijana walijitahidi kucheza kandanda safi hadi dakika ya 27 walipopachika bao la kwanza kupitia kwa Babulu Nusura baada ya kupokea krosi safi ya Abu Selemani. Bao hilo liliwaamsha vijana wa Mchangani ambao waliokuwa wakisaidiwa na upepo na hatimaye mnamo dakika ya 42 wakajipatia bao la kusawazisha. Hadi mapumziko matokeo yalikuwa 1 -1.

The Juniorz wakiwa katika mapumziko


Wakati wa mapumziko ulikuwa ni wakati muafaka kwa vijana kupata ushauri na kurekebisha makosa mawili yaliyojitokeza kipindi cha kwanza. Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kusomana mchezo na pia kujaribu kuona namna wanavyoweza kukutumia mpira mbovu. hadi kipenga cha mwisho kinapulizwa timu hizo ziligawana pointi kwa kutoka sare ya 1 - 1. Matokeo hayo yamewaweka The Juniorz katika nafasi ya pili ya msimao huo wakiwa na pointi 4 na magoli 6.

The Juniorz wakitoka uwanjani

Wakizungumza  baada ya mechi hiyo, wachezaji wote walisikitishwa sana na matokeo ya mechi hiyo kwa kuwa timu waliyocheza nayo haikuwa imejiandaa vyema isipokuwa mpira uliotumika ndio ulisababisha wasipate ushindi mnono hiyo ni kwa sababu kadri muda ulivyozidi kwenda ndio mpira ulivyozidi kuharibika. Hivyo basi walitumia pia fursa hiyo kuwaomba wapenda michezo kwa ujumla kuwasaidia mipira na vifaa vya michezo kwa ujumla ili waweze kushiriki mashindano hayo vizuri na pia kulitwaa kombe hilo.


NA SISI VIONGOZI KWA NIABA YA VIJANA HAWA, TUNAWAOMBA WADAU WOTE KUWAWEZESHA VIJANA HAWA VIFAA VYA MICHEZO KWA KADRI YA UWEZO WENU ILI WATIMIZE NDOTO ZAO ZA KUCHEZA SOKA NA KULISAIDIA TAIFA!!!

Kwa msaada, wasiliana na;
Katibu Mkuu,
Biafra Sports Club (Namba ya Usajili NSC. 9848)
Simu: +255 715 253 653,

TUNAKUSHUKURU SANA!!!



MAZOEZI YA 'JOGGING' YAFANA NA KUWAKUTANISHA WANAMICHEZO TOKA KLABU MBALIMBALI KATIKA FUKWE ZA COCO

Jana (jumapili - 04/05/2012) kama kawaida mazoezi ya mbio za pole pole (jogging) yaliendelea kwa Wanabiafra ambapo mbio zilianzia klabuni 90 Degrees kinondoni kupitia Moroko, Kanisa la Mtakatifu Petro, Shule ya Msingi Oysterbay hadi ufukweni Coco.

Wanabiafra wakiwa katika barabara ya Kawawa kuelekea Moroko

Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi Michael Silili akiongoza msafara


Wanabiafra wakiwa barabara ya Ali Hassan Mwinyi Road maeneo ya Oysterbay Police


Mara baada ya kuwasili ufukweni mazoezi ya viungo yaliendelea kwa kutengeneza duara kubwa na mwelekezaji akiwa katikati ya duara hilo.


(m)duara

Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Ally Masharubu (mwenye jezi Na. 7) akipasha viungo


(m)duara tena


Kutoka kulia ni Mustafa Murro (mwenyekiti kamati ya Nidhamu na Rufaa), Nancy R Rupia (mjumbe Kamati ya Ufundi) na Jaqueline Barozi (Makamu Mwenyekiti)

Wakati mazoezi yakiendelea ufukweni hapo wana-jogging toka klabu ya Msufini nao waliwasili na moja kwa moja na wao waliendelea na mazoezi ya viungo kama ilivyo ada, na mpiga picha wetu alijongea karibu yao na kusaimiana nao na kisha kuendelea kupata picha mbili tatu.

Wana-Msufini Jogging wakifanya Sit-Ups

Muda si mrefu tena wakaingia wana-jogging wa klabu ya Namanga na kufanya jumla ya klabu tatu tofauti za jogging kukutana ufukweni.

Wana-Namanga Jogging wakitengeneza duara

Wanabiafra wakawaelekeza Namanga namna ya kutengeneza mduara kwa haraka

 Mara baada ya kumaliza mazoezi hayo wana Biafra walirudi klabu na moja kwa moja mazoezi ya aerobics yaliendelea kwa zaidi ya dakika 40. Kama kawaida ili aerobics inoge, muziki ni lazima uchagize na mdundo wa wake ndio unaoongoza mazoezi hayo kama wanavyoonekana wanabiafra wakifurahi mazoezi ya aerobics kwa kufuata midundo ya muziki.


Hii inaitwa washa pikipiki style



Gusa kisigino

Wengine wakaamua kucheza muziki kabisa

Makamu Mwenyekiti (Jaqueline Barozi) na Mwenyekiti (Abdul Mollel)


KARIBU UJIUNGE NA BIAFRA SPORTS CLUB KWA MAZOEZI HAYA YA JOGGING KILA JUMAPILI


Thursday, May 03, 2012

MECHI YA KATI YA BIAFRA KIDS NA MCHANGANI FC YAHAIRISHWA

Chama cha mpira wilaya ya Kinondoni (KIFA) ambacho kina ratibu mashindano ya Copa Coca Cola kwa vijana walio chini ya umri wa miaka 17 kimehairisha tena mechi kati ya Biafra Kids na Mchangani FC iliyokuwa ichezwe leo tarehe 3 Mei, 2012 saa 10 jioni katika uwanja wa Kinondoni Muslim. Kuhairishwa kwa mechi hiyo kunatokana na uwanja huo kujaa yatokanayo na mvua inayoendelea kunyesha katika jiji la Dar es Salaam.

Baadhi ya wachezaji wa Biafra Kids

Uongozi wa KIFA umetanabaisha kuwa unajipanga vyema na mapema iwezekanavyo wataujulisha umma wa wapenda maendeleo ya soka juu ya tarehe na mahali mchezo huo utakapopigwa tena.

Wakati huo huo, viongozi na wachezaji wa timu hiyo wameahidi kuitumia fursa hiyo kuendelea na mazoezi kwa ajili ya kujiweka sawa sawa zaidi kimchezo na kimashindano.

Wednesday, May 02, 2012

BIAFRA KIDS YAJIANDAA KUIKABILI TIMU YA MCHANGANI FC TAREHE 3 MEI, 2012

Michuano ya Copa Coca Cola kwa vijana walio chini ya umri wa miaka 17 inaendelea tena juma hili ambapo timu ya Biafra Kids inajitupa tena uwanjani tarehe 3 Mei, 2012 kupambana na timu ya mchangani FC ya Mwananyamala. Mchezo huo utafanyika katika uwanja wa Kinondoni Muslim, Dar es Salaam kuanzia saa 10:00 jioni.  


Baadhi ya wachezaji wa Biafra Kids wakipasha misuli kabla ya kuanza mechi siku walipoitungua African Talent magoli 3 - 1 katika uwanja wa Mwl. Nyerere, Makkurumla.

Akiizungumzia mechi hiyo mara baada ya mazoezi makali yaliyofanyika katika fukwe za Coco hapo jana, nahodha wa timu hiyo Hussein Tahiddin (pichani chini) aliwaonya vijana wa Mchangani wajiandae maana wanafanya mazoezi ya nguvu ili kuhakikisha wanashinda mechi hiyo na zilizobaki na hatimaye kuchukua kombe. Aliwashauri pia vijana wenzake waonyeshe vipaji vyao kwa kuwa wasipoangalia kombaini ya timu ya Kinondoni itaundwa na wachezaji wa Bifra Kids peke yao kwa kuwa wao ndio wanaoonyesha kandanda safi kwenye michuano hiyo. 
Hussein Tahiddin - Nahodha wa Biafra Kids 

Kama kawaida yao viongozi, wanachama na mashabiki wa timu ya Biafra Kids, wameahidi kuwaunga mkono vijana hao kwa kwenda kwa wingi uwanjani kuwashangili na kuwapa hamasa ya ushindi. pia waliwatoa wasiwasi wachezaji wote na kuwaasa wazingatie maelekezo ya walimu na viongozi wao ili kujipatia ushindi kwenye mechi hiyo.

MUNGU IBARIKI BIAFRA KIDS