Tuesday, July 30, 2013

MCHEZO WA MBIO ZA POLE POLE NA USALAMA BARABARANI

"Kuna umuhimu mkubwa sana kwa wana-jogging kutumia vizuri barabara zetu wakati tunapofanya mazoezi ili kupunguza ajali za barabarani". Rai hiyo ilitolewa na Katibu wa Chama cha Jogging Kinondoni ndugu Yahya Poli wakati akitoa salamu za pole kwa wanamichezo wakati wa Msiba wa Bi. Hellen Michael. aliyefariki kwa ajali ya gari wakati akiwa mazoezini.

Ili kuweza kuweza kukimbia barabarani, kuna mambo muhimu ya kuzingatiwa kwa ajili ya usalama wa wakimbiaji Kama yalivyobainishwa hapa chini: - 

1. Kukimbia katika mistari mitatu 
Inashauriwa, kabla ya kuanza mazoezi na kuingia barabara, wanamichezo wote wanapaswa kupanga mistari mitatu iliyonyooka ambapo watoto watapanga mbele ya mistari hiyo. Kupanga mistari mitatu kunawezesha kupunguza usumbufu kwa vyombo vya moto vinavyotumia barabara wakati tukiwa mazoezini. Mara baada ya kupanga na kuanza kuingia barabarani, ni vyema kutumia upande wa kushoto wa barabara. Ni muhimu kwa wakimbiaji wote kuheshimu misari kwa kutoivuruga.
Wakimbiaji wakikimbia katika mistari mitatu

Watoto wakiwa mstari wa mbele kabisa
Angalizo; Kuna uwezekano mkubwa wa kutokea au kusababisha ajali iwapo wanamichezo watakimbia kiholelaholela kwa sababu wanaweza kuzidi hadi upande wa pili wa barabara hivyo kutoa nafasi finyu kwa watumiaji wa vyombo vya moto kupita. Pia, ni rahisi kuwadhibiti watoto wanapokuwa mstari wa mbele.

2. Kuwa na Waongoza na vifaa vya kuongozea
Waongozaji wa mazoezi ni watu muhimu sana kwa kuwa wao kazi yao kubwa ni kuongoza wanamichezo kufuata njia (route) watakayotumia katika maziezi hayo n pia kuongoza vyombo vya moto barabarani. Waongozaji wanapaswa kuwa wawili na kuendelea ambapo mmoja ataongoza mbele ya wanamichezo na mwingine ataongoza nyuma ya wanamichezo. Ili kuboresha usalama, waongozaji wanapaswa kuwa katika umbali kidogo kati yao na wanamichezo na wanapaswa kuwasiliana. Waongozaji pia wanapaswa kuwa na bendera zitakazozuia na kuruhusu vyombo vya moto wakati wa mazoezi.
Muongozaji wa mbele akiwa na kibendera

3. Huduma ya Kwanza
Wakati wote wa mazoezi panapswa kuwepo na huduma ya kwanza. Huduma ya kwanza humsaidia mtu anapopata matatizo kabla ya kumpeleka hospitali. Vikundi vinapaswa kuwa na watoa huduma ya kwanza na kisanduku cha huduma ya kwanza chenye vifaa na dawa mahususi kwa ajili ya utoaji wa huduma ya kwanza.
Mwanamichezo aliyepoteza fahamu mara tu baada ya kumaliza mazoezi
4. Kushirikiana na wadau wa usalama barabarani (trafiki)
Ni vyema kutoa taarifa kwa wadau mbalimbali wa usalama barabarani likiwemo jeshi la polisi idara ya usalama barabarani angalau juma moja kabla ya mazoezi ili wadau hao wapate fursa ya kujipanga na kutoa ushirikiano na msaada pale itakapohitajika kwa haraka na kwa wakati. 

No comments:

Post a Comment