Tuesday, April 23, 2013

TIMU YA SOKA YA VIJANA YA BIAFRA (BYFT) KUCHEZA MECHI YA KIRAFIKI DHIDI YA ETTIHAD FC KATIKA UWANJA WA S/M M'NYAMALA B LEO

Katika kujiandaa na michuano ya Copa Coca Cola na BIafra Cup, timu ya soka ya vijana ya Biafra, leo inakutana na Ettihad FC katika mechi ya kujipima nguvu itakayochezwa katika uwanja wa shule ya msingi Mwananyamala B majira ya saa 10:00 jioni.
Baadhi ya wachezaji wa BYFT wakipasha misuli joto

Golikipa wa BYFT Godwin maarufu Subwoofer


BYFT katika picha ya pamoja na viongozi wao

Shime wadau, wapenzi na mashabiki wa soka hasa la vijana tujitokeze kwa wingi katika kushuhudia mechi hiyo.

Friday, April 19, 2013

NI MUHIMU KUUANDAA MWILI KWA AJILI YA MAZOEZI

Mlezi (Patron) wa klabu ya FAITA JOGGING ndugu Mustafa Mgawe ametukumbusha kwenye ukuta wake wa facebook. Soma hapa chini.

 

Thursday, April 18, 2013

BLOGU YA BIAFRA YATEMBELEWA ZAIDI YA MARA 600 KWA MWEZI MACHI NA APRILI, 2013

Klabu ya michezo ya Biafra  inatoa shukrani kwa watu wote kutoka mataifa mbalimbali duniani kwa kutembelea blogu yake. Katika kipindi cha mwezi mmoja tangu tarehe 20 Machi hadi leo 18 Aprili, 2013 imetembelewa zaidi ya mara 600 na watu kutoka Tanzania, Marekani, Urusi, Uingereza, Oman, Ujerumani, Ufaransa, Brazili, China na Sweden.
Takwimu za leo

Akizungumzia takwimu hizo, Katibu Mkuu wa klabu hiyo ndugu Yahya Poli alibainisha zaidi kwamba blogu hiyo imetembelewa zaidi ya mara 8000 tangu kuanzishwa kwake na pia alitoa wito kwa makampuni na wafanyabiashara kutumia blogu hiyo kutangaza bidhaa zao.

Sunday, April 14, 2013

BIAFRA YAANZA MCHAKATO WA KUANZISHA TIMU YA MPIRA WA PETE

Idara ya wanawake katika Klabu ya Michezo ya Biafra inawahamasisha na kuwaalika wasichana na wanawake wenye vipaji vya mchezo wa mpira wa pete (Netball) na mpira wa miguu kujiunga na klabu na kisha kuanzisha timu. Akizungumza na blogu hii mmoja wa waratibu wa zoezi hilo Bi. Aziza Mwaimu (pichani chini) alibainisha kuwa miongoni mwa wanachama wa klabu hiyo kuna ambao wanapenda kushiriki michezo ya aina mbalimbali hivyo fursa ya kuanzisha timu ni ya kipekee kwao kushiriki michezo
Aziza Mwaimu akionesha kipaji cha kupiga danadana
Makamu M/Kiti wa Biafra Jaqueline Barozi (kulia) akikokota mpira
Kama unapenda kujiunga na timu ya wanawake ya Biafra wasiliana na Katibu Mkuu kwa anuani inayoonekana kwenye kiunganishi upande wa kulia wa blogu hii.

JOGGING YA WANABIAFRA JUMAPILI TAREHE 14 APRILI, 2013 YANOGA

Wanabiafra wengi, wakubwa kwa wadogo leo wamejitokeza mapema asubuhi kwa ajili ya jogging ambayo iliwakusanya pamoja zaidi ya wanamichezo 70. Jogging lianzia klabuni na kuingia barabara ya Kawawa kuelekea Moroko, kisha barabara ya Mwai Kibaki hadi Viktoria kuelekea Mwanayamala hospitali, Mwananyamala A hadi studio, Barabara ya Kawawa tena na kuishia klabuni. Baada ya kufika klabuni wanajogging walifanya 'aerobis kwa zaidi ya dakika 50 kisha kuendelea na shughuli nyingine. Futailia picha chini.
Chris Katembo akiimbisha na kuongoza



Tunawapongeza wanabiafra na wadau wengine wote wlaiojitokeza kwa mazoezi ya leo, tunawakaribisha wengine wengimjiunge na klabu yetu. 

WE, WE, MAZOEZI NI AFYA, ACHA KUJIACHIA!!!

Friday, April 12, 2013

NI UJERUMANI DHIDI YA HISPANIA KATIKA NUSU FAINALI YA LIGI YA MABINGWA ULAYA

Hatimaye nusu fainali ya ligi ya mabingwa ulaya 2013 itazikutanisha timu bora kabisa toka nchini ujerumani na spain. Droo ya nusu fainali hiyo imefanyika leo huko Nyon nchini Uswisi ambapo imedhihirika kuwa vinara wa ligi ya Ujerumani Bayern Munich ambao wanaongoza Bundesliga kwa pointi 75 watamenyana na FC Barcelona wanaoongoza La Liga kwa pointi 78 wakati Borussia Dortmund inayoshika nafasi ya pili Bundesliga ikiwa na pointi 55 itakwaana na Real Madrid ambayo inashika nafasi ya pili pia kwenye La Liga ikiwa na pointi 65.

Mechi ya kwanza katika kinyan'ganyiro hicho itachezwa katika dimba la Allianz Arena nchini Ujerumani ambapo Bayern Munich itawakaribisha FC Barcelona tarehe 23 Aprili, 2013  na siku inayofuata yaani tarehe 24 Aprili, 2013 katika dimba la BVB Stadion Dortmund, Borussia Dortmund itawakaribisha Real Madrid.

Mzunguko wa pili utachezwa tarehe 30 Aprili, 2013 katika uwanja wa Santiago Bernabeu ambapo Real Madrid itaikaribisha  Borussia Dortmund na tarehe 1 May, 2013 katika uwanja wa Camp Nou Barcelona itachuana vikali na Bayern Munich.



Wadau mbalimbali wa soka nchini Tanzania wameanza kubashiri timu zitakazokutana katika fainali ambapo katika ukurasa wake wa Facebook, mwandishi na mchambuzi mahiri wa michezo nchini hususani mchezo wa soka ndugu Shaffih Dauda ambaye pia ni mtangazaji wa kipindi cha michezo cha redio ya Clouds ameandika hivi: - 
 

 Wachezaji wa Timu ya Vijana ya Biafra (BYFT) nao wamebashiri hivyo hivyo katika ukurasa wao wa Facebook ambapo wanatabiri kwamba itaongezeka mechi nyingine ya watani jadi toka nchini hispania (El Classico) kwa mwaka 2013. 
 
Haya, sisi yetu macho, tunasubiri kipute hicho hadi fainali itakayopigwa katika dimba la Wmbley nchini Uingereza.

 

WANABIAFRA WAAZIMIA KUSHIRIKI KATIKA MAFUNZO MBALIMBALI

Wanachama wa klabu ya michezo ya Biafra walikutana katika ukumbi wa 90 Degrees Pub kwa ajili ya mkutano wa kawaida ambapo ajenda kuu ya mkutano huo ilikuwa ni kubaini mahitaji ya mafunzo mbalimbali kwa wanachama wake. Akifungua mkutano huo, Makamu Mwenyekiti wa klagbu hiyo Bi. Jaqueline Barozi (pichani chini) aliwakumbusha wanachama zaidi ya 22 waliohudhuria kikao hicho kuwa jitihada za kutoa mafunzo zina lengo kuwapa fursa wanachama kupata maarifa katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo kwa kadri ya mapenzi yao.
Pia akizungumza katika kikao hicho, katibu mkuu ndugu Yahya Poli aliwakumbusha wadau kuwa kwa mujibu wa Mpango wa Utekelezaji wa Malengo ya Klabu (MUMK) pamoja na Mpango Kazi wa mwaka 2013 klabu imedhamiria kutoa fursa za mafunzo mbalimbali yakiwemo masuala ya ujasiriamali kwa wanachama wake ili waweze kutimiza ndoto na malengo yao ya kujikwamua kiuchumi. 
  
Mara baada ya kikao hicho wanachama waliohudhuria waligawiwa fomu za Kubaini Mahitaji ya Mafunzo kwa Wanachama ili wazijaze na kuzirejesha kwa ajili ya utekelezaji. Kama ungependa kujiunga katika mpango huu wa mafunzo kwa wanachama wa klabu ya michezo ya Biafra, bofya kiunganishi cha "downoload" hapo chini kisha uijaze na kuituma fomu hiyo kwa katibu mkuu katika anuani zinazoonekana kwenye fomu hiyo.

Thursday, April 11, 2013

TAIFA JOGGING YABADILI JINA ILI KUKIDHI MATAKWA YA USAJILI WA KLABU YAO.

Klabu ya michezo ya Taifa Jogging imebadili jina lake kwa mujibu wa ushauri wa msajili wa vyama na vilabu vya michezo Tanzania. Ushauri huo umetokana na klabu hiyo kuwa katika mchakato wa kupata usajili rasmi toka katika Baraza la Michezo Tanzania (BMT). Akizungumza na mwandishi wa habari hii, Mlezi (Patron) wa klabu hiyo bwana Mustafa Mgawe (pichani chini) alisema kwamba kwa sasa klabu hiyo itasajiliwa kwa jina la FAITA JOGGING. Aliendelea kueleza kuwa mchakato wa usajili tayari umeshaanza na unaendelea vizuri.
Viongozi waandamizi wa FAITA JOGGING kutoka kushoto Mrs. Fuime (Mwenyekiti) na Mustafa Mgawe (Mlezi)
Pia Mlezi huyo alitoa rai kwa vilabu vyote vya jogging kuungana na kufuata nyayo za vilabu vya jogging vya manispaa ya Kinondoni ambavyo vipo katika mchakato wa kuanzisha chama cha jogging katika manispaa hiyo. 

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Biafra, ndugu Yahya Poli kwa niaba ya Wanabiafra wote aliwapongeza wana FAITA JOGGING wote kwa ushirikiano walio nao na vilabu vingine na hasa kwa kuanzisha timu ya mpira wa pete (netball) ya wanawake ambayo inajulikana kama FAITA QUEENS. Timu hiyo ilicheza mechi ya kirafiki na timu ya mpira wa pete ya Mzimuni Jogging na kuwafunga.
KIKOSI CHA FAITA QUEENS PICHANI
 

Tuesday, April 09, 2013

UZINDUZI WA KLABU YA MSASANI JOGGING TAREHE 7 APRILI WAFANA

Kama ilivyotolewa taarifa awali, uzunduzi wa klabu ya Msasani Joggiging ulifanyika jumapili tarehe 7 Aprili, 2013 kama ilivyopangwa. Mgeni rasmi katiak uzinduzi alikuwa ni Makamu wa Rais wa Shrikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania ndugu Phares Magesa ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM. Pia uzinduzi huo uliohudhuriwa na wanamichezo zaidi ya mia nane kutoka katika vilabu vya jogging zaidi ya 20, ulihudhuriwa pia na Diwani wa Msasani (viti maalum) Mheshimiwa Christina Kirigiti.

Msasani Jogging wakiongoza Jogging
Baadhi ya klabu zilizoshiriki uzinduzi huo ni Biafra, Namanga, Kunduchi Kwanza, Msufini, Family Jogging, Kawe Social & Sports Club, Kawe Beach Jogging, Kunduchi Jogging, Sotojo, Ukwamani Jogging, Barafu, Mzimuni, Kata 14, Kongowe, Timberland,Unga unga Jogging, Fanja Jogging, Dovya Jogging, n.k. Pichani chini ni baadhi ya vilabu vilivyoshiriki uzinduzi huo vikiwa kwenye jogging.






Mara baada ya jogging iliyokuwa ya takriban kilomita 10 na kuishia katika fukwe za msasani, wanamichezo wote waliendelea mazoezi ya aerobics yaliyokuwa yakiongozwa na ndugu Michael Juma maarufu Mopao kama wanavyoonekana pichani chini.
Punde mgeni rasmi aliwasili eneo la tukio na kupokelewa na Mwenyekiti wa Msasani Jogging ambaye aliambatana na Katibu Mkuu wa Chama cha Jogging Kinondoni ndugu Yahya Poli
Kutoka kulia; Mgeni Rasmi Phares Magesa, M/kiti Msasani Jogging na Katibu Mkuu Yahya Poli
Katika hotuba yake ya uzinduzi huo, mgeni rasmi aliwaasa wanamichezo kutumia pia fursa zinazowaunganisha pamoja katika michezo kwa ajili ya kujiletea maendeleo ya kiuchumi  na kwa kuonesha mfano alichangia shilingi laki tatu kwenye mfuko wa Msasani Jogging Club ili waweze kuanzisha biashara na wadau mbalimbali walioshiriki uzinduzi huo nao walichangia.
Mgeni rasmi Phares Magesa akiwahutubia wanamichezo
Uzinduzi huo pia uliambatana na burudani mbalimbali ambapo wanamichezo walipata fursa ya kujumuika na kuburudika pamoja. 

Klabu ya Michezo ya Biafra inatoa pongezi kwa wanachama wote wa Msasani Jogging kwa kufanikisha uzinduzi wa klabu yao na kuwasisitiza kuimarisha yao kwa kufuata malengo yaliyopelekea kuanzishwa klabu hiyo.

Friday, April 05, 2013

TFF YAZINDUA MPANGO WA MAENDELEO 2013-2016; MAONI YA BIAFRA KUHUSU MPANGO HUO.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limezindua rasmi Mpango wa Maendeleo wa Mpira wa Miguu (Technical Development Plan- TDP) wa 2013-2016 ambao pamoja na mambo mengine unahusisha kutazama upya mfumo wa mashindano na kuunda kanda kwa ajili ya kusimamia maendeleo.

Uzinduzi huo umefanywa leo (Aprili 4 mwaka huu) na Rais wa TFF, Leodegar Tenga katika hafla iliyofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na washirika mbalimbali wakiwemo wachezaji, viongozi wa mpira wa miguu, Serikali, klabu na Wahariri wa Michezo.

Rais Tenga amesema mpango huo unafuatia ule wa 2004-2007, na 2008-2012 ambayo ilitengenezwa kwa msaada wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA). Mpango wa sasa umetengenezwa na TFF kwa kufuata mpango mfano (standard plan) wa FIFA.

Amesema mpango wa sasa ni wa kiufundi zaidi kwa vile umelenga kuendeleza mpira wa miguu, kwani iliyotangulia ilihusisha zaidi kutengeneza muundo wa TFF, kazi ambayo imekamilika kwani sasa shirikisho lina vyombo mbalimbali vya kusimamia mchezo huo.

Wakati ule tulikuwa na Ligi Kuu tu, lakini tumeongeza mashindano ya aina mbalimbali kama U17, U20, Kombe la Taifa na sasa michuano ya Copa Coca-Cola itakuwa ya U15. Pia tukatengeneza Kanuni za Fedha, kilichomo katika mpango wa sasa ni kujenga mpira. Chombo (TFF) tayari kipo,” amesema.

Rais Tenga amesema TFF imefika hapa kutokana na watu kujitolea ambapo ametaka moyo huo uendelezwe, lakini akasisitiza washirika wote kuwa na mpango huo na kuusoma kwani umetokana na maoni yao ambapo kila mmoja ana kazi ya kufanya katika mpango huo.

Naomba washirika wote wasome mpango huu. Kama mtu una mawazo zaidi baada ya kusoma, toa maoni yako. Mpango huu si Msahafu, utabadilika kutokana na maoni ya watu. Kama una mawazo zaidi, toa maoni yako kwa lengo la kujenga, isiwe kazi ya kulaumu tu kuwa mpango una upungufu. Mabadiliko yanafanyika kutokana na mawazo mapya,” amesema.

Amesema maendeleo ya mpira wa miguu ni mchakato mrefu, kwa hiyo unahitaji ushiriki wa watu kutokana na ukweli kuwa uongozi wa mpira wa miguu Tanzania bado ni wa kujitolea.
 
Rais Tenga amesema ahadi ya TFF ni kushirikiana na washirika mbalimbali kuhakikisha kuna maendeleo kwa faida ya mpira wa miguu wenyewe na nchi kwa ujumla.

Amewashukuru wote waliotoa maoni kwa ajili ya mpango huo wenye kurasa 76. Mpango huo ulioandaliwa na Mkufunzi wa FIFA, Henry Tandau, Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Sunday Kayuni na Ofisa Maendeleo wa TFF, Salum Madadi unapatikana kwenye CD na nakala laini (soft copy).

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

MAONI YETU;
Klabu ya Michezo ya Biafra inatoa pongezi kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kuandaa na kuuzindua mpango huo wa maendeleo wa miaka mitatu (2013/16). Maoni yetu kwa TFF ni kuzidi kushirikisha wadau mbalimbali katika utekelezaji wa mpango huo. Kwa mfano, TFF imeongeza mashindano ya kama U17, U20, Kombe la Taifa na sasa michuano ya Copa Coca-Cola itakuwa ya U15, basi ni vyema kutoa taarifa za michuano hiyo kwa wakati na bila upendeleo ili timu mbalimbali zinazostahili (qualify) ziweze kushiriki katika mashindano hayo.

MAANDALIZI YA UZINDUZI WA KLABU YA MSASANI JOGGING TAREHE 7 APRILI, 2013 YAKAMILIKA

Zimebaki siku mbili tu kabla ya tukio kubwa la kimichezo, hasa linaohusisha mchezo wa mbio za pole pole kutokea ambapo klabu ya mchezo huo inayojulikana kama Msasani Jogging inatarajiwa kuwakutanisha zaidi ya wana-jogging 700 kutoka katika vilabu takriban 20 vya mkoa wa Dar es Salaam na Pwani kushiriki katika uzinduzi huo. Taarifa ya Katibu Mkuu wa klabu ya Msasani Jogging ndugu Mangula inatanabaisha zaidi.
Katibu Mkuu wa Msasani Jogging Bwana Mangula akichangia harambee Kunduchi
Akizungumza na mwandishi wa blogu hii Bwana Mangula alieleza kwamba katika uzinduzi huo klabu takriban20 zimealikwa na kuthibitisha kushiriki na kuzitaja klabu hizo kuwa ni Biafra, Namanga, Barafu, Mzimuni, Kata 14, Kongowe, Timberland, Kawe Jogging, Kawe Beach, Ukwamani, Unga unga Jogging ya Kawe, Kunduchi Kwanza Jogging, Kunduchi Jogging, Fanja Jogging ya Msasani, Msufini Jogging na Dovya Jogging
 


Bwana Mangula alifafanua zaidi kwamba, uzinduzi huo utatanguliwa na mbio za pole pole zitakazowashirikia wanamichezo wote na zitaanzia maeneo ya CCBRT Msasani kuelekea Namanga hadi Mbuyuni kuelekea kanisa la mtakatifu Petro hadi shule ya msingi Oysterbay, mbio zitaendelea hadi katika fukwe za Coco kuelekea barabara ya Chole hadi Msasani Mwisho barabara ya kuelekea soko la samaki la msasani na kuishia katika fukwe za Msasani ambapo michezo mbalimbali ya ufukweni itafanyika na baadaye wanamichezo wote watajumuika pamoja katika uzinduzi rasmi

Pia, alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wadau na wanamichezo wote. 




Tuesday, April 02, 2013

KUELEKEA ROBO FAINALI YA LIGI YA MABINGWA ULAYA LEO TAREHE 2 APRILI, 2013 PSG v BARCELONA NA BAYERN MUNICH v JUVENTUS

Kipute cha kuanza kwa mikikimikiki ya hatua ya robo fainali ya ligi ya mabingwa Ulaya (UCL) 2012/13 kinaanza leo usiku majira ya saa 3:45 (kwa saa za afrika mashariki) wakati  mwamuzi Wolfgang Stark  kutoka nchini Ujerumani atakapopuliza kipyenga katika mechi inayowakutanisha wababe ambao ni vinara katika ligi za nchi zao Paris Saint German (PSG) watakapowakaribisha Barcelona (Barca) katika uwanja wa Parc des Princes ndani ya jiji la Paris na pia kutazamwa na mamilioni ya mashabiki wa soka duniani kote.

PSG ambao ndio wenyeji katika mpambano huo watakuwa wakiongozwa na kocha wao Carlo Ancelotti ambaye anatarajiwa kuchezesha kikosi chake mahiri kuanzia kwa mlinda mlango Sirigu; Jallet, Thiago Silva, Alex, Maxwell; Matuidi, Verratti; Moura, Lavezzi, Pastore; Ibrahimovic
Silaha za maangamizi za PSG kutoka kushoto David Beckham, Jeremy Menez na Zlatan Ibrahimovic
 Baada ya kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kwa ajili ya matibabu ya ugonjwa wa saratani, kocha wa Barcelona, Tito Vilanova leo ataongoza benchi la ufundi la timu hiyo ambapo kikosi chake kinatarajiwa kuwajumuisha mlinda mlango Valdes; Alves, Mascherano, Pique, Alba; Xavi, Busquets, Iniesta; Sanchez, Messi na Villa. Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, mshambuliaji wa timu hiyo David Villa (pichani chini) alisisitiza kutorudia kosa walilofanya Milan.
Wakati huo huo katika uwanja wa Allianz-Arena uliopo mjini Munich, Ujerumani, Bayern Munich wataikaribisha Juventus ya Italia katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa robo fainali ya michuano ya ligi ya klabu bingwa ulaya. Mtanange huo unatarajiwa kuchezeshwa na mwamuzi kutoka nchini Uingereza Mark Clattenburg. Kocha wa Bayern Munich - Jupp Heynckes (pichani chini) akizungumza na wandishi wa habari alitanabaisha kwamba wachezaji wote wako tayari kwa mechi hiyo na wana ari kubwa ya ushindi.
Kocha wa Bayern Munich - Jupp Heynckes
Heynckes anatarajiwa kuwachezesha Manuel Neuer, Dante, Jerome Boateng, Daniel Van Buyten, Philip Lamn, Holger Badstuber, Franck Ribery, Arjen Robben, Thomas Muller, Bastian Schweinsteiger na Mario Mandzukic katika kikosi cha kwanza.

Antonio Conte (pichani chini) kocha wa Juventus akiizungumzia mechi hiyo aliwaonya wenyeji wao kwa kuwaarifu kuwa wanakwenda Munich wakiwa tayari wanahisi ni majeruhi na wanachofuata ni ushindi wakiwa ugenini
Antonio Conte
Conte anatarajiwa kuchezesha kikosi chake hatari cha maangamizi ambacho kinaongozwa na Gianluigi Buffon, Giorgio Chiellini, Martin Caceres, Leonardo Bonucci, Andrea Barzagli, Andrea Pirlo, Sebastian Giovinco, Kwadwo Asamoah, Arturo Vidal, Claudio Marchisco and Mirko Vucinic. 

Picha zote zimepakuliwa toka vyanzo mbalimbali mtandaoni.

MATUKIO YA JOGGING JUMAMOSI TAREHE 30 MACHI, 2013

Kanuni ya kufanya mazoezi siku ya jumapili kwa wanabiafra ilitenguliwa rasmi baada ya kushirikiana na Namanga Jogging kufanya mazoezi ya pamoja siku ya jumamosi tarehe 30 Machi, 2013 ili kutoa fursa kwa wanachama wa vilabu hivyo ambao ni wakristo kuhudhuria ibada ya asubuhi ya Jumapili ya pasaka. Mazoezi hayo yaliyoandaliwa na kuratibiwa na klabu ya Namanga, yalianza na kuishi Leecarz Pub ambapo ni makao makuu ya Namanga Jogging. Fuatilia picha hapa chini.
Wanajogging wakikatiza barabara ya Ally Hassan Mwinyi kuelekea Leaders Club