Sunday, April 29, 2012

BIAFRA KIDS YASHINDA MECHI YAKE DHIDI YA AFRICAN TALENT

Kinyang'anyiro cha mashindano ya Copa Coca Cola chini ya miaka 17 wilaya ya Kinondoni kimeendelea tena leo katika uwanja wa Mwl. Nyerere, Magomeni Makurumla kwa kuzikutanisha timu za Biafra Kids dhid ya African Talent. Mechi hiyo iliyokuwa ichezwe majira ya saa 10 jioni ilichezwa saa 5 asubuhi kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo waandaaji.
Biafra Kids wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa klabu ya michezo ya Biafra muda mfupi kalba ya kuanza mechi

Mechi hii, wachezaji walipania sana kushinda baada ya kupoteza mchezo wao wa kwanza dhidi ya Eleven Boys kwa magoli 4 - 1. Hivyo walifanya mazoezi ya nguvu na kujiongezea ari kubwa ya ushindi na hatimaye kuichabanga timu ya African Talent kwa mabao 3 - 1.


Biafra Kids katika picha ya pamoja na wanachama na mashabiki

 Hamasa ya ushindi pia ilichangiwa na mashabiki wengi waliofunga safari kuja kuishangilia timu hiyo. kama picha inavyojieleza hapo juu, wanachama na mashabiki hao hawakujali mvua iliyokuwa ikinyesha bali walichohitaji ni ushindi tu na si vinginevyo. Mashabiki hao wake kwa waume waliishangilia timu yao tangu mwanzo hadi mwisho wa mchezo.
Biafra Kids - kikosi kilichoanza (first eleven) katika picha ya pamoja


Wachezaji wakipasha misuli kabla ya kuingia uwanjani


 Mfungaji wa goli la kwanza Abu Selemani (wa kwanza kushoto) na mfungaji goli la tatu Khamis Ibrahim (wa katikati)


Mabeki Machachari wa Biafra Kids Fareed Massoud (kushoto), Ahmad Ibraheem (kulia) na Abdul Moshi (nyuma)


tayari kwa ukaguzi na kuanza kwa mechi


Timu mwenyeji wa mechi hiyo African Talent wakisalimiana na Biafra Kids


Manahodha wa timu zote mbili katika picha ya pamoja na refa wa mchezo huo


Biafra Kids wakilisakama lango la African Talent

Karamu ya magoli ilifunguliwa na Abuu Selemani dakika ya 18 baada ya kupokea krosi safi ambapo aliiunganisha nyavuni na kumwacha kipa wa African Talent akiruka bila kuupata mpira. Baada ya kufunga tu goli hilo, kasi ya mchezo ilingezeka maradufu na mnamo dakika ya 24 Babulu Hamad aliipatia Biafra Kids bao la pili. African talent walijipatia bao la kufutia machozi kwa njia ya penati baada ya mchezaji wao kujidondosha katika eneo la hatari na kumhadaa refa kuwa amechezewa rafu . Dakika ya 41 karamu ya magoli ilihitimishwa na Khamis Ibrahim ambaye aliutia mpira nyavuni kiufundi. 

Mara baada ya nusu ya kwanza ya mchezo kukamilika, Biafra Kids walitanza soka la ukweli na kusababisha kosa kosa kadhaa na magoli ambayo refa aliyakataa.

Biafra Kids inatarajia kujitupa tena uwanjani tarehe 1 Mei, 2012  kuchuana na Vijana Muslim pale pale kwenye uwanja wa Mwl. Nyerere.

MUNGU IBARIKI TIMU YETU!

Thursday, April 26, 2012

BIAFRA KIDS YACHEZA MECHI YA KWANZA YA MICHUANO YA COPA COCACOLA CHINI YA UMRI WA MIAKA 17

Michuano ya kuwania kombe la Copa Cola kwa vijana walio chini ya umri wa miaka 17 imeanza leo ambapo katika uwanja wa Mwl. Nyerere Magomeni Makurumla timu ya soka ya Biafra Kids ilimenyana na timu ya Eleven Boys.
Kikosi cha kwanza cha Biafra Kids - The Juniors

 Katika mchezo huo timu ya Biafra Kids imepoteza kwa kufungwa goli 4 -2 matokeo yaliyipa changamoto timu hiyo kuongeza bidii ya mazoezi na mbinu mbalimbali za kimchezo ambapo imeonekana dhahiri kuwa timu kadhaa zimesajili wachezaji wenye umri wa zaidi ya miaka 17 kama inajielekeza ligi hiyo.

Biafra Kids pamoja na Eleven Boys wakikaguliwa

Hadi mapumziko tumi hizo zilikuwa zimetoka sare ya 1 - 1 ambapo mchezaji machachari wa timu hiyo Jimmy Elvis Juma ndiye aliyeipatia bao la kufutia machozi.

Mfungaji wa goli la Biafra Kids Jimmy E. Juma

Kipindi cha pili kilikuwa kigumu kwa timu ya Biafra Kids ambapo vijana wa Eleven Boys waliongeza mabao mengine mawili na Biafra Kids kupitia kwa mshambuliaji wake hodari Mashaka Masumbwi walijipatia bao la kufutia machozi.
mjumbe wa kamati ya Utendaji, Henry Maseko (kushoto) na Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi, Michael Silili (kulia) wakiwa na mfungaji wa goli la kufutia machozi, Mashaka Masumbwi (katikati)

Wakizungumza baada ya kumalizika kwa mechi hiyo, viongozi, wanachama na mashabiki wa klabu ya michezo ya Biafra walionyesha kuridhishwa na kiwango cha wachezaji kwenye mechi hiyo na pia walipata fursa ya kutoa nasaha zao kwa wachezaji, viongozi na hata mashabiki kwa ujumla. Makamu Mwenyekiti wa klabu Bi. Jackline M. Barozi aliwaahidi vijana hao klabu itawasapoti katika kila hatua na kuwasihi waongeze bidii ili mechi zijazo zote tushinde na hatimaye kuchukua kombe.

Baadhi ya wachezaji wa Biafra Kids wakiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya ufundi
Baada ya kupokea nasaha vijana waliahidi kufanyia marekebisho makosa yote yaliyobainishwa na kuwahakikishia wanachama kwamba kombe hili la kopa coca cola litabaki mikononi mwao. Pia walibainisha mahitaji muhimu ili kuweza kukamilisha ndoto yao ya kucheza soka na miongoni mwa mahitaji hayo ni vifaa vya michezo kama vile jezi kwa ajili ya mechi na mazoezi, koni, viatu, soksi, n.k.

Kikosi cha Biafra Kids kilichocheza leo katika picha ya pamoja na mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi, Michael Silili (wa kwanza kushoto waliosimama) na mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Henry Maseko (wa mwisho kulia waliosimama)

Timu hiyo inajitupa tena katika uwanja wa Mwl. Nyerere, Magomeni Makurumla, jumapili tarehe 29, Aprili 2012 saa 10:00 jioni kuchuana na timu ya African Talent hivyo wamewaomba viongozi, mashabiki na wanachama kuwaunga mkono kwa kuwapatia vifaa vya michezo na kwenda kwa wingi kweny mechi kuwashangilia na kuwapa hamasa ya ushindi.

Monday, April 23, 2012

TANZIA

Juma lililopita, klabu ya Biafra ilipata taarifa za msiba toka kwa mwanachama wake na mjumbe wa kamati ya Uchumi na Mipango ya klabu Bi. Mariam Sabaje ambaye amefiwa na kaka yake juma lililopita huko mkoani Mbeya. Mipango ya mazishi inafanyika huko huko Mbeya na Bi. Mariam Sabaje amesafiri Ijumaa ili kuhudhuria msiba huo.
Bi. Mariam Sabaje ( mwenye suruali nyeupe) akiwa pamoja na wanachama wa Biafra

Viongozi, wanachama na mashabiki wa Biafra wanatoa pole kwa mwanachama mwenzao pamoja na familia yake kwa ujumla. Tuko pamoja! Kama ilivyo ada, rambirambi zinaendelea kukusanywa ili tumkabidhi mwanachama mwenzetu na kumpa mkono wa pole. 
Bi. Mariam Sabaje akisherehesha klabuni

BWANA AMETOA! BWANA AMETWAA! JINA LAKE LIHIMIDIWE

Tuesday, April 17, 2012

Biafra Kids in Scoring Motion

Wakiwa katika maandalizi ya kushiriki michuano ya Copa Cocacola (chini ya umri wa miaka 17) 2012. Hebu tujikumbushe goli maridadi lililofungwa na Biafra Kids aka The Juniors (wenye jezi za blue) dhidi ya Simba Kids


Friday, April 13, 2012

TANZIA

Katika juma hili klabu inasikitika kutangaza misiba miwili mfululizo. Katika msiba wa kwanza Mweka Hazina wa klabu Bi. Asha Mweke Warisanga (pichani chini) amefiwa na kaka yake huko Nairobi nchini Kenya. Msiba huo ulitokea mwanzo mwa juma hili na kwa sasa Mweka Hazina huyo yuko Nairobi kwa ajili ya kushiriki maziko.
MRS. ASHA M. WARISANGA - MWEKA HAZINA WA BIAFRA SPORTS CLUB

 Pia mnamo majira ya jioni ya tarehe 12 Aprili, 2012 ilitolewa taarifa ya msiba wa baba mzazi wa mwanachama mwingine wa klabu Bi. Upendo Kimaro. Kwa mujibu wa Upendo (pichani chini), Mzee Kimaro amefariki huko Arusha na yeye yuko kwenye maandalizi ya kuhudhuria msiba huo mapema iwezekanavyo.
UPENDO KIMARO
Klabu inatoa pole na kutuma salamu za rambirambi kwa wanachama wake hao pamoja na familia zao kwa ujumla. Tuko pamoja katika kipindi hiki kigumu cha msiba na majonzi makubwa kwa kupoteza ndugu zetu. Tunamuomba Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema azilaze roho za marehemu mahala pema peponi - Amen

BWANA AMETOA, BWANA AMETWAA, JINA LAKE LIHIMIDIWE

Thursday, April 12, 2012

KAMATI MBALIMBALI ZA KLABU ZAKUTANA KUJADILI UTEKELEZAJIA WA MAJUKU YA KAMATI HIZO

Kuanzia siku ya Jumanne tarehe 10 hadi 13 Aprili, 2012 kamati mbalimbali za klabu ya michezo ya Biafra zitakuwa zikikutana kwa ajili ya kujadili na kujipanga juu ya utekelezaji wa majukumu mbalimbali yanayozigusa kamati hizo. Kwa mujibu wa katibu mkuu wa klabu hiyo ndugu Yahya Poli (Kaka Poli) kamati ya kwanza kabisa kukutana ilikuwa ni kamati ya Uchumi na Mipango ambayo ilikutana Jumanne tarehe 10 Aprili, 2012 Baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo ni ndugu Ibrahim Kilasa, Robert Mwakibugi, Mariam Sabaje na Maneno Juma pamoja na masuala mengine walijadili juu ya fursa mbalimbali zilizopo ambazo zinaweza kuleta maendeleo ya kiuchumi kwa klabu, wanachama wake na jamii kwa ujumla. Pia kamati hiyo iliazimia kuandaa mpango mkakati wa utekelezaji wa majukumu yao.
Ibrahim Kilasa - Mjumbe wa kamati ya Uchumi na Mipango

Kamati ya Nidhamu na Rufaa ilikutana tarehe 11 Aprili, 2012 ambapo wajumbe wa kamati hiyo baadhi yao ni Mustapha Muro, Ismail Hamad, Mwajuma Usale, Adam Mwambapa na Emmy Jack ambapo kamati hiyo pamoja na masuala mengine ilianza kuainisha masuala mbalimbali ya kinidhamu na kubainisha baadhi ya vipengele vya kanuni za adhabu.  Kamati hiyo pia inaanda mpango kazi wake.

Emmy Msechu (mwenye kilemba) - Mjumbe wa Kamati ya Nidhamu na Rufaa 

Alhamisi, Aprili 12, 2012 Kamati ya Ufundi inakutana ambapo kamati hiyo, pamoja na masuala mengine itajadili na kutengeneza mpango wake. Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo ni Michael Silili, Ramadhani Said, Ally Juma, Nancy Raphael na Acholo Luvanda.

Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Ufundi - Ally Juma (mwenye tracksuit nyekundu), Ramadhani Said (wa nne kutoka kushoto) na Michael Silili (mwenye tracksuit nyeusi)

Kamati ya Utendaji inatarajia kukutana tarehe 13 Aprili, 2012. Katika kikao hicho wenyeviti wa kamati zote tatu watashiriki na kuwasilisha kwa muhtasari waliyoyajadili na kuazimia kwenye vikao vyao. Maazimio hayo yatajumuishwa katika mpango kazi wa kamati ya utendaji na baadaye kuwasilishwa kwa wanachama wote.

Baadhi ya wajumbe wa kamati ya Utendaji kutoka kulia - Jacqueline Barozi (Makamu Mwenyekiti), Henry Maseko, Abdul Mollel (Mwenyekiti) na Yahya Poli (Katibu Mkuu)

Tuesday, April 10, 2012

FURAHA NGANDA ASHINDA PAMBANO LAKE DHIDI YA JAMHURI SAIDI TAREHE 8 APRILI, 2012

"Nimefurahi sana kwa ushindi huu, nilimwambia Jamhuri (Said) ajiandae vya kutosha, hakunielewa, alifikiri namtania, sasa nimemuonesha kuwa mimi si wa kawaida, si wale wale, hapa kazi tu". Hayo ni maneno ya Mwanamasumbwi Furaha Nganda mara baada ya kumaliza pambano lake na bondia machachari Jamhuri Saidi katika ukumbi wa Dar Live Mbagala.

Furaha Nganda (mwenye bukta ya bluu akimsukumia konde zito Jamhuri Said (Picha zote kwa hisani ya Super D)


Mpambano kati ya mabondia hao ulikuwa ni wa utangulizi ambapo pambano lenyewe hasa liliwakutanisha mabondia Rashid Matumla (Snake Boy) dhidi ya Manano Oswald (Mtambo wa Gongo) ambapo Maneno Oswald alishinda pambano hilo na kunyakua ngao ya pasaka. kwa matokeo ya mpambano huo na mapambano mengineyo duniani tembelea tovuti ya Boxing Records.

Viongozi na wanachama wote wa Biafra Sports Club wanampongeza Mwanabiafra mwenzao Furaha Nganda kwa ushindi huo na kumsisitiza aongeze bidii kwenye mazoezi na kutunza afya yake! 

Friday, April 06, 2012

MWANABIAFRA FURAHA NGANDA KUZIPIGA DAR LIVE TAREHE 8 APRILI, 2012

Kwa wapenzi na mashabiki wa mchezo wa ndondi aka ngumi, aka masumbwi aka mtifuano basi jumapili hii ya tarehe 8 Aprili, 2012 kuanzia saa 10 jioni basi tusikose kwenda kumshuhudia mwanamasumbwi machachari Furaha Nganda (pichani chini) atakapopanda ulingoni kuwawakilisha vyema wanabiafra apmoja na wakaazi wote wa Kinondoni atakapomchakaza mwanadada Jamhuri Said  katika ukumbi wa Dar Live Mbagala. Akizungumzia mpambano huo Furaha alikuwa na haya ya kusema "nawasisitiza wanakinondoni mje kwa wingi kunshangilia maana nakwenda kufanya kazi na si vinginevyo. Nahitaji raudni tatu tu kuangaza ushindi maana 'KO' ndio kitu ninachokifahamu."

FURAHA NGANDA

Thursday, April 05, 2012

BIAFRA KIDS YAJIDHATITI KUSHIRIKI KOMBE LA COPA COCA COLA 2012 WILAYA YA KINONDONI

Klabu ya michezo ya Biafra imeiingiza timu yake ya watoto inayojulikana kama Biafra Kids a.k.a. The Juniors katika kinyan'ganyiro cha kuwania kombe la Copa Cocacola -2012 ambalo linatarajiwa kuanza juma lijalo. Akiongea kwa kujiamini nahodha wa Timu hiyo Tajuddin Hussein alisema kuwa wamejiandaa kushiriki kikamilifu na kuchukua kombe la Copa Cocacola wilaya ya Kinondoni kwani wameshiriki katika ligi mbalimbali na kuchukua vikombe na sasa ni wakati muafaka kwa timu yao kushiriki michauano mikubwa kama ya Copa Cocacola.



KIKOSI CHA BIAFRA KIDS KILIPOCHEZA NA KOMBAINI YA TIMU YA WATOTO WANAOISHI KATIKA MAZINGIRA MAGUMU AGOSTI, 2011

 Pia wachezaji wa timu hiyo wamewaomba mashabiki wa timu yao na mchezo wa mpira wa miguu kwa ujumla kuwaunga mkono na kuwasaidia kwa hali na mali katika kufanikisha ushiriki wa timu hiyo kwenye michuano ya Copa Cocacola wilaya Kinondoni.

KIKOSI CHA BIAFRA KIDS KILIPOCHEZA NA TIMU YA WATOTO YA SIMBA
FOMU YA USAJILI WA TIMU YA BIAFRA KIDS  ILIYOWASILISHWA TFF

Wednesday, April 04, 2012

WATU WENGI WAJITOKEZA KUPATA ELIMU YA SARATANI YA TEZI DUME PAMOJA NA UPIMAJI WA SARATANI HIYO TAREHE 25 MACHI, 2012

Pale katika ukumbi wa Leecars Pub, Namanga jijini Dar es Salaam palikuwa na shughuli ya utoaji elimu ya saratani ya tezi dume ambayo hujulikana pia kama saratani ya kibofu cha mkojo kwa wanaume ambapo utolewaji huo wa elimu uliambatana upimaji wa saratani hiyo.

Baadhi ya wanamichezo walioshiriki katika zoezi la upimaji na elimu ya saratani ya tezi dume



ICHAGUE BLOGU YA BIAFRA KATIKA TUZO ZA BLOGU ZA TANZANIA - 2012


Blogu ya klabu ya michezo ya Biafra ambayo tangu iwe hewani kwa mara ya kwanza kwa kubisha hodi mnamo mwezi Agosti, 2011 imekuwa hai na kuweka habari mbalimbali za kimichezo na afya zinazoihusu klabu ya Biafra pamoja na klabu nyingine . Mpaka tunapoandika hapa leo, blogu imeshatembelewa zaidi ya mara 1900 na watu kutoka nchi mbalimbali duniani na wengi zaidi wanazidi kuitembelea kila siku.

Baadhi ya wanabiafra wakiwa katika mazoezi ya mbio za pole pole (jogging)


Hivyo basi, klabu inapenda kuchukua fursa hii kukuomba wewe mwanachama, shabiki, mpenzi na mdau wa blogu pamoja na michezo kwa ujumla kuipigia kura blogu yetu katika 'kategori' 3 ambazo ni Blogu ya Mwaka, Blogu Mpya na Blogu ya Michezo katika Tuzo za Blogu za mwaka 2012 kwa kujaza Fomu ya Kuichagua Blogu.

Makamu Mwenyekiti wa Biafra Jaqueline Barozi (wa kwanza kushoto) na Mweka Hazina (mwenye fulana nyekundu) wakijadiliana na wanachama.

KURA YAKO NI MUHIMU SANA!!!!